Msuva: Kiatu cha Dhahabu kinanihusu

WAKATI Yanga ikianza msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania bara kwa kusuasua, ‘habari ya mjini’ iliyowala katika midomo ya mashabiki wa soka nchini ilikuwa ni usajili wa klabu hiyo wa wachezaji wao wa Kibrazil, Genilson Santos ‘Jaja’ na Andrey Coutinho.
Yanga walikumbana na kipigo cha 2-0 dhidi ya Mtibwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambako hawajapata ushindi kwa zaidi ya misimu mitano sasa katika ligi.
Lakini kipigo hicho kilitanguliwa na ushindi mnono wa 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii ya utamaduni wa kufungua ligi dhidi ya mabingwa wa msimu uliopita Azam FC.
Na mechi hiyo ndiyo hasa iliyochochea umaarufu wa Jaja, ambaye alifunga magoli mawili likiwamo kali la kuuinua mpira juu ya kipa wa Azam, Mwadini Ali, ambaye alibaki ameganda kama amepigiliwa msuri akikosa cha kufanya wakati akishuhudia mpira ukitinga wavuni.
Wakati vichwa vya habari vikiwa ni Jaja, kuna mchezaji mmoja ambaye kuingia kwake uwanjani akitokea benchini ndiko hasa kulikoiamsha Yanga hadi kupata ushindi huo mnono.

SIMON MSUVA
Msimu uliopita, mshambuliaji wa pembeni Msuva alikuwa muhimu sana Yanga akianza mara kwa mara, lakini kutua kwa kocha mpya Mbrazil Maximo kumeonekana “kumsahau” mkali huyo.
Akitumika kama mshambuliaji wa akiba au ‘super sub’, Msuva amethibitisha tena na tena umuhimu wake kikosini humo kwa kuitumia vyema nafasi anayopewa bila ya kumwangusha mwalimu wake.
Kuingia kwa Msuva dhidi ya Azam kuliwanyima usingizi mabeki wa mabingwa hao, akahusika katika kila hatari na kufunga goli moja katika ushindi huo mnono.
Bao hilo lilimpa heshima ya kipekee Msuva kwa mashabiki wa Yanga na lilimfanya kuwa kivutio cha aina yake na kuwafanya mashabiki kumshangilia kwa muda wote.
Mechi ya kwanza ya ligi haikuwa njema kwa Yanga ambao walilala 2-0 mjini Morogoro, lakini walizinduka katika mechi ya pili na kupata pointi tatu za kwanza kwenye kwa ushindi wa 2-1, ushindi ambao hata hivyo kocha wa Prisons, David Mwamaja aliulalamikia akimtupia lawama mwamuzi wa mchezo huo akimtuhumu kuwa aliwabeba sana Yanga na kuwanyima Prisons zaidi ya penalti tatu za wazi.
Mabao ya Yanga yalipatikana kupitia kwa kiungo Mbrazili Countinho ambaye alipiga mpira wa adhabu ambao ulienda moja kwa moja wavuni na bao la pili lilipatikana kupitia kwa Msuva ambaye aliunganisha kwa kichwa maradadi mpira wa krosi.
Msuva aliondoka kama shujaa katika mechi hiyo kwa mambo makubwa mawili. Kwanza mechi ilikuwa ngumu sana kwa Yanga, kwani licha ya Prisons kubaki 10 uwanjani kutokana na kadi nyekundu, walikuwa wanacheza kwa nguvu kubwa na waliutawala mchezo kwa muda mwingi hasa katika kipindi cha pili.
Jambo la pili ni kuwa Yanga walikuwa wanahitaji ushindi kwa namna yeyote ili kurudisha imani kwa mashabiki wake, ikizingatiwa kwamba walikuwa wamepoteza mechi yao ya kwanza ya ligi mbele ya Mtibwa Sugar, lakini pia walipata bao la mapema huku mchezaji wa Prisons akipata kadi nyekundu lakini bado Prisons wakarejesha bao hilo wakiwa pungufu na wakawa wanasaka bao la ushindi kwa nguvu kubwa.
Hii ilibeba maana kubwa kwa bao la pili la Yanga lililofungwa na Msuva kwa Wanajangwani walipata nguvu mpya tena kubwa na Prisons wakadhoofika kidogo kutokana na bao lenyewe kufungwa katika dakika za lala salama.
Kufunga magoli mawili katika mechi tatu (ikiwamo ya Ngao ya Jamii) kunadhihirisha kauli ya Msuva kwamba amedhamiria kufanya makubwa msimu huu katika mbio za kuwania kuibakisha nchini nchini tuzo ya Kiatu cha Dhahabu ya Mfungaji Bora wa ligi baada ya msimu uliopita kiatu kuchukuliwa na mchezaji wa kigeni, Amissi Tambwe wa Simba.
Msuva aliiambia NIPASHE kuwa ndoto zake ni kuona siku moja anashinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu, na atafurahi zaidi kama jambo hilo litawezekana msimu huu.

BENCHI SIYO HATARI
Wakati msimu umeanza huku Msuva akionekana kuwa si chaguo la kwanza la Maximo, mshambuliaji huyo anasema ataongeza juhudi mazoezini na kujaribu kufanya makubwa katika nafasi atakazopewa na kocha kwenye mechi ili kumshawishi Mbrazil huyo.
“Nina furaha hapa, tena hata mwalimu anavyonichezesha nafurahia sana, ananipa mbinu nikiwa benchi, na nazitumia napata magoli muhimu. Mechi yetu dhidi ya Prisons ilikuwa ngumu sana ila mimi nilichokifanya niliangalia wanavyocheza, nikatazama upungufu wao ndiyo maana nilipoingia nikapata goli muhimu la ushindi,” anasema.
“Mechi ni ngumu. Unaweza kuona wachezaji na benchi la ufundi wanavyochanganyikiwa na kujaribu kuweka mambo sawa. Mashabiki wanahitaji ushindi kutoka kwetu, hawataki kuona tunaendelea kupoteza au kupata sare, wanachotaka ni ushindi tu. Sisi kama wachezaji tunafurahia hali hiyo ya mashabiki kutupa presha ya kuhitaji matokeo kwani inatusukuma kupambana zaidi, na hii ina manufaa kwa klabu yetu.
“Ninahitaji kuwa mfungaji bora ndo maana kasi yangu kwa sasa ipo kwenye magoli najua kuna wachezaji wengi ni wazuri hapa, tukicheza kitimu lazima nitafunga sana na hatimaye nitaibuka na Kiatu cha Dhahabu,” alisema Msuva.
Kuhusiana na mwenendo wa ligi kuu bara baada ya Yanga kucheza mechi za awali, Msuva anasema kuwa ligi ya sasa ni ngumu na yenye ushindani mkubwa na klabu ndogo ambazo zimepnda daraja zimekuwa zikicheza kwa nguvu huku zikikamia mechi dhidi ya timu kubwa.
“Tuna kazi kubwa sisi tunaocheza klabu kubwa, klabu nyingi zimepania na zinapenda kuifunga Yanga yenye wachezaji wenye majina makubwa, ila hilo halitupi shida tunajua tuna kazi kubwa ya kufanya na hatutaangalia kuwa tunacheza dhidi ya nani, kila mechi tutaweka jitihada na kuonyesha kiwango bora,” anasema.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s